Jumamosi 21 Novemba 2026 - 22:15
Wimbi la maandamano ya vijana katika bara la Ulaya; kupinga gharama za maisha, matumizi ya kijeshi na sera za serikali

Hawza/ Makumi ya maelfu ya vijana na wananchi katika nchi mbalimbali za Ulaya wamejitokeza mitaani kuandamana kupinga sera za kijeshi, kupanda gharama za maisha, mgogoro wa makazi na kupungua uwekezaji katika huduma za umma. Waandamanaji, wakibeba kaulimbiu ya kutetea mustakabali wa kizazi cha vijana, wametaka maandamano hayo yaendelee.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, sambamba na kuongezeka kutoridhika wananchi katika nchi za Ulaya, vijana katika takribani nchi 20 za bara hilo wameandaa maandamano na migomo iliyoratibiwa kwa pamoja, wakieleza kupinga kwao ongezeko la matumizi ya kijeshi, kupanda gharama za maisha, mgogoro wa makazi na hali isiyoridhisha ya huduma za umma.

Maandamano hayo yalianza siku ya Ijumaa, Novemba 20, kwa kaulimbiu isemayo: "Tupiganie mustakabali wetu, siyo vita vyao." Yanatarajiwa kuendelea pia katika siku za Novemba 21 na 22. Vyama vya wafanyakazi, jumuiya mbalimbali pamoja na mashirika ya wanafunzi wa shule na vyuo vikuu ni miongoni mwa waandaaji wa harakati hizo za maandamano.

Nchini Italia, makumi ya maelfu ya watu waliandamana katika miji ya Roma na Milan. Chama cha Wafanyakazi cha CGIL kilitangaza kufanyika kwa mikusanyiko takribani 100 katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, iliyoshirikisha zaidi ya watu milioni moja.

Waandamanaji hao, sambamba na kupinga ongezeko la bajeti ya silaha na gharama za maisha, walitaka kufanyiwa mabadiliko sera za kiuchumi na kijamii za serikali.

Nchini Ujerumani, kundi la "GenZ regelt" lilitangaza kuwa takribani watu 21,000 walishiriki katika maandamano yaliyofanyika katika miji 70. Takribani vijana 1,000 walikusanyika mjini Berlin kupinga mwenendo wa kuongeza silaha na uwezekano wa kurejeshwa utaratibu wa utumishi wa kijeshi wa lazima.

Waandamanaji hao pia walisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika sekta ya elimu na kupinga kupunguzwa bajeti ya huduma za umma.

Nchini Ufaransa, sambamba na kuadhimisha mwaka wa nane tangu kuanzishwa vuguvugu la "Gilets Jaunes" (Mavazi ya Njano), mamia ya vijana waliandamana mjini Paris kupinga kuongezeka kwa siasa za kijeshi katika jamii na kutetea mustakabali wa kizazi cha vijana.

Nchini Hispania, mamia ya watu mjini Madrid waliandamana kupinga ongezeko la matumizi ya kijeshi, huku wakitaka kuimarishwa elimu ya umma na kuboreshwa hali ya vituo vya elimu.

Nchini Uingereza, mamia ya watu, wakiwemo wanafunzi wa shule, walikusanyika mjini London wakiwa na kaulimbiu isemayo: "Tupiganie mustakabali wetu, siyo vita vyao."

Mbali na kupinga sera za kijeshi, waandamanaji hao walionya kuhusu madeni ya mikopo ya elimu yanayowakabili vijana, mgogoro wa nishati, kuongezeka gharama za maisha na athari za mgogoro wa tabia nchi.

Sambamba na maandamano hayo, vyama vya wafanyakazi na mashirika yanayojihusisha na masuala ya makazi kutoka nchi saba za Ulaya, ambazo ni Ubelgiji, Uingereza, Hispania, Ufaransa, Ugiriki, Italia na Ureno, viliwasilisha madai sita ya pamoja.

Madai hayo ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa makazi kwa kila mtu, kupunguza bei za bidhaa na huduma, kuongeza mishahara, kutoza kodi matajiri na kukomesha sera za kuongeza silaha.

Mwanahistoria wa Ufaransa, Sylvain Boulouque, akizungumzia sifa za kipekee za maandamano hayo, ameeleza kuwa uratibu wake katika ngazi ya Ulaya ni jambo linalostahili kuzingatiwa. Amesisitiza kuwa mojawapo ya mambo yanayounganisha maandamano hayo ni wananchi kutokuwa na imani na vyombo vya polisi na watu wenye mamlaka.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa, maandamano hayo hayatakoma baada ya kumalizika kwa wiki hii. Nchini Ubelgiji pia, migomo na mikusanyiko mingine ya maandamano imepangwa kufanyika siku ya Jumatatu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha